(1 Yohana 3, Marko 2, Kumbukumbu la
Torati 28, Luka 9)
Somo hili limetafsiriwa
kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko
yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978,
1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu
kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa
Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye
mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine
yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea
somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata
kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com
kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org
kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa,
Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Je, ungependa washiriki waongezeke zaidi
kanisani kwako? Huo ndio mjadala unaoendelea kanisani kwangu hivi sasa! Watu wana
mawazo ya kufanya utandaaji, lakini mimi wazo langu ni kwamba “Hebu tufanye
juhudi za kuwaponya wagonjwa!” Je, umewahi kufikiria kwamba hiyo ni njia nzuri
ya kuwaleta washiriki wapya kanisani kwako? Hiyo ndio njia aliyoitumia Yesu, si
ndio? Au, je, alitumia njia gani? Je, Yesu aliwaponya watu ili ayavute makundi
makubwa ya watu kumsikiliza, au aliwaponya watu kwa sababu aliwahurumia? Endapo
unawaponya watu ili kuwavutia watu wengine kuisikiliza injili, je, huko sio
kuonesha huruma? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tuone kile
tunachoweza kujifunza juu ya kukabiliana na ugonjwa!
I.
Mioyo na Uponyaji
A.
Soma 1 Yohana 3:16-18. Wangapi kati yenu wanapendelea
kuonesha upendo kwa maneno? (Kwa sababu gharama yake ni ndogo, hutumia muda
mfupi, na kuna maumivu kidogo!)
1.
Je, Biblia inatuasa kuwa tuonesheje upendo? (“Kwa matendo
na kweli.”)
a.
Je, kauli ya “kwa kweli” inamaanisha nini katika huu
muktadha? (Inamaanisha kwamba kutenda jambo fulani kunafanya matendo yako ya
upendo yawe ya kuaminika.)
B.
Soma 1 Yohana 3:19-20. Je, inamaanisha nini kwa “mioyo
yetu kutuhukumu?” (Inamaanisha kujisikia hatia.)
1.
Je, Biblia inatuambia nini katika haya mafungu
tuliyojifunza? (Tunatakiwa kuonesha upendo si kwa maneno tu. Tutajisikia vizuri
kwa kuwasaidia watu walio wahitaji.)
C.
Je, mafungu haya yanaashiria nini kwenye maswali
niliyoyauliza kwenye utangulizi? Endapo tunaweza kufanya uponyaji kuwa sehemu
ya uinjilisti kwa njia ya utandaaji, je tunapaswa kufanya hivyo? (Ndiyo! Bila kujali
kama unafanya uponyaji ili kuvutia makundi ya watu kuisikiliza injili, au
unawaponya wale ambao tayari wameshavutiwa na injili, unaonesha kujihusisha
kwako kwenye pande zote mbili za wahusika – hali ya kiroho na ya kimwili.)
D.
Soma 1 Yohana 3:21-22. Je, umeuona uponyaji kanisani
kwako?
1.
Kama hujauona, je, fungu hili linaashiria nini? (Kwamba
tunaweza kuuomba uponyaji.)
2.
Je, ahadi hii ina masharti yoyote? (Inasema kuwa
tunaweza kupokea jambo lolote tuliombalo endapo tunamtii Mungu.)
E.
Soma 1 Yohana 3:23. Je, tunazungumzia utii wa aina
gani? (Kumwamini Yesu na kuwapenda watu wengine. Hii inaashiria kuwa tunatakiwa
kuyapa kipaumbele maombi kwa ajili ya uponyaji (kumwamini Mungu) kwa niaba ya
watu maalum (kuwapenda wengine).)
F.
Soma 1 Yohana 3:24. Je, tunakaaje ndani ya Yesu na Yesu
anakaaje ndani yetu? (Hii ni rejea mahsusi ya Roho Mtakatifu kukaa ndani yetu
na sisi kuishi maisha yanayoendana na matakwa ya Roho Mtakatifu. Hili ni jambo
la muhimu sana.)
G.
Hebu tuwe wakweli kabisa kwa dakika chache. Jambo gani
linafanya kuwasaidia watu wengine liwe na maumivu? Hivi punde tu nimesema kuwa
kuwasaidia watu wengine kunatufanya tujisikie vizuri. Je, ni yote mawili?
1.
Je, unaweza kubainisha nyakati ambazo ulijisikia vizuri
kuwasaidia watu wengine na nyakati ambazo ulijisikia vibaya? Je, jambo gani
linaleta utofauti? (Kutatua tatizo kwa mtu mwenye shukrani kunafanya mtatuzi wa
tatizo ajisikie vizuri. Tatizo la kudumu lisilotatulika linalomhusisha mtu
asiye na shukrani huleta maumivu/hukatisha tamaa kwa mtatuzi wa tatizo.)
2.
Je, Yesu alishughulikaje na matatizo ya watu
waliomwendea? (Alitatua matatizo yao mara moja. Hebu tuangalie mfano katika
sehemu inayofuata.)
II.
Yesu na Uponyaji
A.
Soma Marko 2:1-3. Je, watu wanakuja kwa ajili ya
kusikiliza neno au kwa ajili ya uponyaji? (Yote mawili. Lakini inaonekana kama
vile watu wengi zaidi wanakuja kwa ajili ya kusikiliza maneno ya Yesu.)
B.
Soma Marko 2:4. Endapo ungekuwa unazungumza na
makutano, je, ungependa kumwona mtu akitoboa dari kwenye mahali ambapo
unazungumza na watu?
1.
Je, ungependa kuona mtu akishushwa kupitia katikati ya
watu? (Litakuwa jambo la kuvuruga usikivu wa watu.)
C.
Soma Marko 2:5. Je, Yesu anarejea imani ya nani?
(Inaonekana kama anarejea imani ya kundi la watu waliomshusha, na sio tu imani
ya yule mgonjwa, kwa kuwa kauli ya Yesu inasema, “imani yao.”)
1.
Jiweke kwenye nafasi ya mmojawapo wa wale wasaidizi
wanne. Je, Yesu anasema maneno ambayo ulikuwa unatarajia kuyasikia? (Hapana! Mwenzangu
amepooza. Nisingekuwa na haja ya kumpitishia darini na kumshusha hadi chini kwa
ajili ya kusamehewa dhambi. Ninataka Yesu amponye.)
a.
Je, inawezekana kwamba Yesu anazungumzia dhambi ya
kuingilia wasilisho/mazungumzo yake?
D.
Soma Yohana 9:1-3. Je, swali la wanafunzi linafunua
nini juu ya fikra za watu kuhusu dhambi na ugonjwa? (Mambo yote mawili
yanahusiana.)
1.
Je,Yesu anafanya hitimisho juu ya hii imani maarufu?
(Anafanya hivyo kwenye hili suala pekee. Hajibu kuwa, “Mnasema nini, hivi
mmekuwa wendawazimu?” Badala yake, anasema kuwa hapa si dhambi za wazazi wala
za mtoto zilizochangia kwenye tatizo.)
2.
Je, unafikiria nini juu ya sababu aliyoitoa Yesu?
a.
Kumbuka kisa cha Ayubu na marafiki wake? Marafiki wa
Ayubu walimwambia Ayubu kuwa alikuwa akiteseka kwa sababu ya dhambi zake. Je,
jibu analolitoa Yesu kuhusu mtu kipofu linahusika kwenye muktadha wa Ayubu?
(Ndiyo!)
E.
Hebu turejee kwenye kisa chetu juu ya mtu
aliyepitishiwa darini. Soma Marko 2:6-8. Je, waandishi wako sahihi? (Ndiyo,
Mungu ndiye anayesamehe dhambi.)
1.
Kama waandishi wako sahihi, kwa nini Yesu anawauliza?
(Kwa sababu hili ni suala tata kwa miaka mingi – je, Yesu ni Mungu?
F.
Soma Marko 2:9-12. Hebu tupitie maswali tuliyoyaibua
hapo awali. Kwa nini Yesu alitenda huu uponyaji? (Inaonekana sababu kubwa ni
kuthibitisha kuwa yeye ni Mungu.)
1.
Endapo tutamwomba Roho Mtakatifu awaponye watu ili
tuweze kuwaleta watu kanisani, je, hiyo itakuwa sababu thabiti? (Tunataka
kuwaongoa watu ili watambue kwamba Yesu ni Mungu.)
2.
Je, ni sababu gani nyingine zinazoashiriwa kwa huu
uponyaji? (Angalia tena Marko 2:5. Yesu alihamasishwa na imani yao.)
a.
Je, jambo hili linatufundisha nini kuhusu mpango wa
kutumia uponyaji ili kuiendeleza injili? (Tunatakiwa kuwa na imani. tunatakiwa
kuiombea.)
b.
Kutokana na kisa hiki, unadhani tunaweza kufanya hivi
kanisani kwetu? Je, tungeweza kufanya uponyaji endapo tungekuwa na uwezo wa
Roho Mtakatifu? (Fikra ya kawaida inaweza kuwa ni mtego. Angalia njia ya
marafiki isiyo ya kawaida. Hawakumwambia rafiki wao, “Hatuwezi kufanya hivi
leo, watu ni wengi sana.” Badala yake, mmoja wao alipendekeza, “Hebu tupande
darini na tutoboe tundu analoweza kupita mtu ili tuweze kuingilia wasilisho la
Yesu kwa kukuweka mbele yake. Nadhani Yesu atatupatia thawabu kwa jambo hili!”
Hiyo ni imani, sio mantiki.)
G.
Soma Kumbukumbu la Torati 28:15 na Kumbukumbu la Torati
28:20-22. Je, watu walikuwa sahihi kufikiria kwamba kuna uhusiano kati ya dhambi
na ugonjwa? (Ndiyo, kabisa. Ninaona angalao sababu tatu kuu za ugonjwa: a)
Tunaishi kwenye dunia yenye dhambi; b) Kushindwa kwetu wenyewe; na, c) Kumpa
Mungu utukufu. Mara nyingine sababu zote tatu zinaonekana kuhusika.)
III.
Uponyaji na Utandaaji
A.
Soma Luka 9:1-2. Kama kuna uhusiano kati ya dhambi na
ugonjwa, je, “tunawaponya” watu kwa kuwaongoa? (Ndiyo!)
1.
Je, hii ndio njia ya kuliendeleza kanisa? (Tunaonesha
ubunifu wa fikra tunapoliendeleza kanisa kwa kusema kuwa endapo unamfuata Yesu
utakuwa mwenye afya njema, na maisha yako yatakuwa bora.)
B.
Mojawapo ya mambo mazuri kuhusu mimi kufundisha katika
Chuo Kikuu cha Regent ni kwamba walimu na wanafunzi wengi ni sehemu ya kile
ninachokiita Ukristo wa “Utakatifu wa Kipentekoste.” Hawa ni Wakristo wanaochukulia
suala la utii kwa Mungu na uwezo wa Roho Mtakatifu kwa umakini sana. Utagundua kwamba
Luka 9:1 inawazungumzia wanafunzi “Kumi na Wawili.” Je, uponyaji ulitengwa kwa
ajili yao au katika kipindi chao? (Soma Yohana 14:12-14. Fungu hili linasema
kuwa “mambo makubwa” yanawezekana kwa “yeyote aniaminiye.” Katika mafungu
machache yanayofuatia (Yohana 14:16-17) Yesu anaahidi kutupatia Roho Mtakatifu
ili akae pamoja nasi. Uponyaji unawezekana kwa njia ya uwezo wa Roho Mtakatifu.)
C.
Soma 1 Wakorintho 12:8-9. Je, hii inatufundisha nini?
(Mambo mawili. Uponyaji ni karama ya Roho. Pili, Mungu ni mkuu (mwenye enzi). Anaamua
ampatie nani karama na nani aponywe.)
D.
Soma Ufunuo 21:3-4. Je, hatma ya ahadi ya uponyaji ni
ipi? (Wale watakaookolewa wataishi kwenye dunia itakayofanywa upya, mahali ambapo
kifo, maumivu na ugonjwa vitakuwa ni mambo ya zamani. Sifa kwa Mungu!)
E.
Rafiki, Mungu anaweza kukupatia karama ya Roho wa
uponyaji, lakini hata kama hakukupatia, unao uwezo wa kuwaambia watu wengine
habari za Yesu. Uhusiano na Yesu unatusaidia kuepuka kujiletea ugonjwa na
unatupatia ahadi ya kuwa na dunia isiyo na dhambi na ugonjwa. Kwa nini
usishiriki habari hizi na watu wengine leo?
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.